Agano la Kale

Agano Jipya

Luka 19:20-33 Biblia Habari Njema (BHN)

20. “Mtumishi mwingine akaja, akasema: ‘Chukua fedha yako; niliificha salama katika kitambaa,

21. kwa maana niliogopa kwa sababu wewe ni mtu mkali. Wewe ni mtu ambaye huchukua yasiyo yako, na kuchuma ambacho hukupanda.’

22. Naye akamwambia: ‘Nakuhukumu kutokana na msemo wako, ewe mtumishi mbaya! Ulijua kwamba mimi ni mtu mkali, ambaye huchukua yasiyo yangu na kuchuma nisichopanda.

23. Kwa nini, basi, hukuiweka fedha yangu benki, nami ningeichukua pamoja na faida baada ya kurudi kwangu?’

24. Hapo akawaambia wale waliokuwa pale: ‘Mnyanganyeni hiyo fedha, mkampe yule aliyepata faida mara kumi.’

25. Nao wakamwambia: ‘Lakini Bwana, huyo ana faida ya kiasi hicho mara kumi!’

26. Naye akawajibu: ‘Kila aliye na kitu atapewa na kuzidishiwa. Lakini yule asiye na kitu, hata kile alicho nacho kitachukuliwa.

27. Na sasa, kuhusu hao maadui zangu ambao hawapendi niwe mfalme wao, waleteni hapa, mkawaue papa hapa mbele yangu.’”

28. Yesu alisema hayo, kisha akatangulia mbele yao kuelekea Yerusalemu.

29. Alipokaribia kufika Bethfage na Bethania, karibu na mlima wa Mizeituni, aliwatuma wanafunzi wake wawili,

30. akawaambia: “Nendeni katika kijiji kilicho mbele yenu. Mtakapokuwa mnaingia kijijini, mtamkuta mwanapunda amefungwa ambaye hajatumiwa na mtu. Mfungueni, mkamlete hapa.

31. Kama mtu akiwauliza kwa nini mnamfungua, mwambieni, ‘Bwana anamhitaji.’”

32. Basi, wakaenda, wakakuta sawa kama alivyowaambia.

33. Walipokuwa wanamfungua yule mwanapunda, wenyewe wakawauliza, “Kwa nini mnamfungua mwanapunda huyu?”

Kusoma sura kamili Luka 19