Agano la Kale

Agano Jipya

Luka 19:11-29 Biblia Habari Njema (BHN)

11. Wakati watu walipokuwa bado wanasikiliza hayo, Yesu akawaambia mfano. Hapo alikuwa anakaribia Yerusalemu, na watu wale walidhani kwamba muda si muda, ufalme wa Mungu ungefika.

12. Hivyo akawaambia, “Kulikuwa na mtu mmoja wa ukoo wa kifalme aliyefanya safari kwenda nchi ya mbali ili apokee madaraka ya ufalme, halafu arudi.

13. Basi, kabla ya kuondoka, aliwaita watumishi wake kumi, akawapa kiasi cha fedha kila mmoja na kuwaambia: ‘Fanyeni nazo biashara mpaka nitakaporudi.’

14. Lakini wananchi wenzake walimchukia na hivyo wakatuma wajumbe waende wakaseme: ‘Hatumtaki huyu atutawale.’

15. “Huyo mtu mashuhuri alirudi nyumbani baada ya kufanywa mfalme, na mara akaamuru wale watumishi aliowapa zile fedha waitwe ili aweze kujua kila mmoja amepata faida gani.

16. Mtumishi wa kwanza akatokea, akasema: ‘Bwana, faida iliyopatikana ni mara kumi ya zile fedha ulizonipa.’

17. Naye akamwambia: ‘Vema; wewe ni mtumishi mwema. Kwa kuwa umekuwa mwaminifu katika jambo dogo, utakuwa na madaraka juu ya miji kumi!’

18. Mtumishi wa pili akaja, akasema: ‘Bwana, faida iliyopatikana ni mara tano ya zile fedha ulizonipa.’

19. Naye akamwambia pia: ‘Nawe utakuwa na madaraka juu ya miji mitano.’

20. “Mtumishi mwingine akaja, akasema: ‘Chukua fedha yako; niliificha salama katika kitambaa,

21. kwa maana niliogopa kwa sababu wewe ni mtu mkali. Wewe ni mtu ambaye huchukua yasiyo yako, na kuchuma ambacho hukupanda.’

22. Naye akamwambia: ‘Nakuhukumu kutokana na msemo wako, ewe mtumishi mbaya! Ulijua kwamba mimi ni mtu mkali, ambaye huchukua yasiyo yangu na kuchuma nisichopanda.

23. Kwa nini, basi, hukuiweka fedha yangu benki, nami ningeichukua pamoja na faida baada ya kurudi kwangu?’

24. Hapo akawaambia wale waliokuwa pale: ‘Mnyanganyeni hiyo fedha, mkampe yule aliyepata faida mara kumi.’

25. Nao wakamwambia: ‘Lakini Bwana, huyo ana faida ya kiasi hicho mara kumi!’

26. Naye akawajibu: ‘Kila aliye na kitu atapewa na kuzidishiwa. Lakini yule asiye na kitu, hata kile alicho nacho kitachukuliwa.

27. Na sasa, kuhusu hao maadui zangu ambao hawapendi niwe mfalme wao, waleteni hapa, mkawaue papa hapa mbele yangu.’”

28. Yesu alisema hayo, kisha akatangulia mbele yao kuelekea Yerusalemu.

29. Alipokaribia kufika Bethfage na Bethania, karibu na mlima wa Mizeituni, aliwatuma wanafunzi wake wawili,

Kusoma sura kamili Luka 19