Agano la Kale

Agano Jipya

Luka 18:27-43 Biblia Habari Njema (BHN)

27. Yesu akajibu, “Yasiyowezekana kwa binadamu, yanawezekana kwa Mungu.”

28. Naye Petro akamwuliza, “Na sisi, je? Tumeacha vitu vyote tukakufuata!”

29. Yesu akawaambia, “Kweli nawaambieni, mtu yeyote aliyeacha nyumba au mke au ndugu au wazazi au watoto kwa ajili ya ufalme wa Mungu,

30. atapokea mengi zaidi wakati huu wa sasa, na uhai wa milele wakati ujao.”

31. Yesu aliwachukua kando wale kumi na wawili, akawaambia, “Sikilizeni! Tunakwenda Yerusalemu na huko kila kitu kilichoandikwa na manabii kuhusu Mwana wa Mtu kitakamilishwa.

32. Kwa maana atakabidhiwa kwa watu wa mataifa nao watamtendea vibaya na kumtemea mate.

33. Watampiga mijeledi na kumuua; lakini siku ya tatu atafufuka.”

34. Lakini wao hawakuelewa jambo hilo hata kidogo; walikuwa wamefichwa maana ya maneno hayo, na hawakutambua yaliyosemwa.

35. Wakati Yesu alipokaribia Yeriko, kulikuwa na mtu mmoja kipofu ameketi njiani akiomba.

36. Aliposikia umati wa watu ukipita aliuliza, “Kuna nini?”

37. Wakamwambia, “Yesu wa Nazareti anapita.”

38. Naye akapaza sauti akisema, “Yesu, Mwana wa Daudi, nihurumie!”

39. Wale watu waliotangulia wakamkemea wakimwambia anyamaze; lakini yeye akazidi kupaza sauti: “Mwana wa Daudi, nihurumie!”

40. Yesu alisimama, akaamuru wamlete mbele yake. Yule kipofu alipofika karibu, Yesu akamwuliza,

41. “Unataka nikufanyie nini?” Naye akamjibu, “Bwana, naomba nipate kuona.”

42. Yesu akamwambia, “Ona! Imani yako imekuponya.”

43. Na mara huyo kipofu akapata kuona, akamfuata Yesu akimtukuza Mungu. Watu wote walipoona hayo, wakamsifu Mungu.

Kusoma sura kamili Luka 18