Agano la Kale

Agano Jipya

Luka 16:1-17 Biblia Habari Njema (BHN)

1. Yesu aliwaambia wanafunzi wake: “Tajiri mmoja alikuwa na karani wake. Huyu karani alichongewa kwamba alitumia ovyo mali ya tajiri wake.

2. Yule tajiri akamwita, akamwambia: ‘Ni mambo gani haya ninayosikia juu yako? Toa hesabu ya mapato na matumizi ya mali yangu, kwa maana huwezi kuwa karani tena.’

3. Yule karani akafikiri: ‘Bwana wangu amenifukuza kazi ya ukarani; nitafanya nini? Kwenda kulima siwezi; kwenda kuombaomba kama maskini ni aibu.

4. Naam, najua la kufanya, ili nitakapofukuzwa kazi, watu waweze kunikaribisha nyumbani kwao.’

5. Basi, akawaita wadeni wa bwana wake, mmojammoja, akamwambia yule wa kwanza: ‘Unadaiwa kiasi gani na bwana wangu?’

6. Yeye akamjibu: ‘Mapipa 100 ya mafuta ya zeituni.’ Yule karani akamwambia: ‘Chukua hati yako ya deni, keti haraka, andika hamsini.’

7. Kisha akamwuliza mdeni mwingine: ‘Wewe unadaiwa kiasi gani?’ Yeye akamjibu: ‘Magunia 100 ya ngano.’ Yule karani akamwambia: ‘Chukua hati yako ya deni, andika themanini.’

8. “Basi, yule bwana akamsifu huyo karani asiye mwaminifu, kwa kuwa alitumia busara. Kwa maana watu wa dunia hii wana busara zaidi na mambo yao kuliko watu wa mwanga.”

9. Naye Yesu akaendelea kusema, “Nami nawaambieni, jifanyieni marafiki kutokana na mali ya dunia, ili zitakapowaishieni, wawapokeeni katika makao ya milele.

10. Yeyote aliye mwaminifu katika mambo madogo, atakuwa mwaminifu katika mambo makubwa; na yeyote asiye mwaminifu katika mambo madogo, hatakuwa mwaminifu katika mambo makubwa.

11. Kama basi, nyinyi si waaminifu kuhusu mali mbaya za dunia, ni nani atakayewakabidhi zile mali za kweli?

12. Na kama nyinyi si waaminifu kuhusu mali ya mtu mwingine, ni nani atakayewakabidhi mali yenu wenyewe?

13. “Hakuna mtumishi awezaye kuwatumikia mabwana wawili; kwa maana atamchukia mmoja na kumpenda mwingine, au ataambatana na mmoja na kumdharau mwingine. Hamwezi kumtumikia Mungu na mali pamoja.”

14. Lakini Mafarisayo waliposikia hayo, kwa vile wao walikuwa wanapenda sana fedha, wakamdharau Yesu.

15. Hapo akawaambia, “Nyinyi mnajifanya wema mbele ya watu, lakini Mungu anaijua mioyo yenu. Kwa maana kile kinachoonekana kuwa kitukufu mbele ya watu, Mungu anakiona kuwa takataka.

16. “Sheria na maandishi ya manabii vilikuwako mpaka wakati wa Yohane Mbatizaji. Tangu hapo, ufalme wa Mungu unahubiriwa, na kila mmoja anauingia kwa nguvu.

17. Lakini ni rahisi zaidi mbingu na dunia kupita, kuliko hata herufi moja ya sheria kufutwa.

Kusoma sura kamili Luka 16