Agano la Kale

Agano Jipya

Luka 15:7-18 Biblia Habari Njema (BHN)

7. Kadhalika nawaambieni, ndivyo kutakavyokuwa na furaha mbinguni kwa ajili ya kutubu kwa mwenye dhambi mmoja, kuliko kwa ajili ya watu tisini na tisa wanaojiona kuwa wema, wasiohitaji kutubu.

8. “Au mwaonaje? Tuseme mwanamke fulani ana sarafu kumi za fedha, akipoteza moja, atafanya nini? Atawasha taa, ataifagia nyumba na kuitafuta kwa uangalifu mpaka aipate.

9. Akiipata, atawaita rafiki na jirani zake na kusema, ‘Furahini pamoja nami, kwa sababu nimeipata ile sarafu yangu iliyopotea.’

10. Kadhalika nawaambieni, ndivyo watakavyofurahi malaika wa Mungu kwa sababu ya mwenye dhambi mmoja anayetubu.”

11. Yesu akaendelea kusema, “Kulikuwa na mtu mmoja mwenye watoto wawili wa kiume.

12. Yule mdogo alimwambia baba yake: ‘Baba, nipe urithi wangu.’ Naye akawagawia mali yake.

13. Baada ya siku chache, yule mdogo aliuza urithi wake, akasafiri na fedha aliyopata, akaenda nchi ya mbali ambako aliitumia ovyo.

14. Alipomaliza kutumia kila kitu, kukatokea njaa kali katika nchi ile, naye akaanza kuhangaika.

15. Akaomba kazi kwa mwananchi mmoja wa huko naye akampeleka shambani mwake kulisha nguruwe.

16. Alitamani kula maganda waliyokula wale nguruwe, ila hakuna mtu aliyempa kitu.

17. Alipoanza kupata akili, akafikiri: ‘Mbona kuna wafanyakazi wengi wa baba yangu wanaokula na kusaza, nami ninakufa njaa?

18. Nitarudi kwa baba yangu na kumwambia: Baba, nimemkosea Mungu, na nimekukosea wewe pia.

Kusoma sura kamili Luka 15