Agano la Kale

Agano Jipya

Luka 12:36-51 Biblia Habari Njema (BHN)

36. muwe kama watumishi wanaomngojea bwana wao arudi kutoka harusini, ili wamfungulie mara atakapobisha.

37. Heri yao watumishi wale ambao bwana wao atakaporudi atawakuta wanakesha! Nawaambieni hakika, huyo bwana atajifunga mkanda kiunoni, atawaketisha mezani na kuwahudumia.

38. Hata kama atarudi usiku wa manane au alfajiri na kuwakuta wanakesha, heri yao watumishi hao!

39. Jueni kwamba, kama mwenye nyumba angejua saa ambayo mwizi atakuja, angekesha, wala hangeiacha nyumba yake ivunjwe.

40. Nanyi, kadhalika muwe tayari, maana Mwana wa Mtu atakuja saa msiyoitazamia.”

41. Petro akamwambia, “Bwana, mfano huo ni kwa ajili yetu tu, au ni kwa ajili ya watu wote?”

42. Bwana akajibu, “Ni nani, basi, aliye mtumishi mwaminifu na mwenye busara, ambaye bwana wake atamweka juu ya watumishi wake ili awape chakula wakati ufaao?

43. Heri yake mtumishi huyo ikiwa bwana wake atakaporudi atamkuta akifanya hivyo.

44. Hakika atampa madaraka juu ya mali yake yote.

45. Lakini, kama mtumishi huyo akijisemea moyoni: ‘Bwana wangu amekawia sana kurudi;’ kisha akaanza kuwapiga watumishi wenzake, wa kiume au wa kike, na kula, kunywa na kulewa,

46. bwana wake atarudi siku asiyoitazamia na saa asiyoijua; atamwadhibu mtumishi huyo vibaya na kumweka fungu moja na wasioamini.

47. Mtumishi ambaye anajua matakwa ya bwana wake lakini hajiweki tayari kufanya anavyotakiwa, atapigwa sana.

48. Lakini yule afanyaye yanayostahili adhabu bila kujua, atapigwa kidogo. Aliyepewa vingi atadaiwa vingi; aliyepewa vingi zaidi atadaiwa vingi zaidi.

49. “Nimekuja kuwasha moto duniani; laiti ungekuwa umewaka tayari!

50. Ninao ubatizo ambao inanipasa niupokee; jinsi gani ninavyohangaika mpaka ukamilike!

51. Mnadhani nimekuja kuleta amani duniani? Hata kidogo; si amani bali utengano.

Kusoma sura kamili Luka 12