Agano la Kale

Agano Jipya

Luka 12:3-15 Biblia Habari Njema (BHN)

3. Kwa hiyo, kila mliyosema gizani, watu watayasikia katika mwanga, na kila mliyonongona faraghani milango imefungwa, yatatangazwa juu ya nyumba.

4. “Nawaambieni nyinyi rafiki zangu: Msiwaogope wale wanaoua mwili, wasiweze kufanya kitu kingine zaidi.

5. Nitawaonesheni yule ambaye ni lazima kumwogopa: Mwogopeni yule ambaye baada ya kuua ana uwezo wa kumtupa mtu katika moto wa Jehanamu. Naam, ninawaambieni, mwogopeni huyo.

6. Inajulikana kwamba shomoro watano huuzwa kwa sarafu ndogo kumi, au sivyo? Lakini mbele ya Mungu hasahauliki hata mmoja.

7. Lakini hata nywele za vichwa vyenu zimehesabiwa zote. Msiogope, basi; nyinyi mna thamani kuliko shomoro wengi!

8. “Nawaambieni kweli, kila mtu anayekiri hadharani kwamba yeye ni wangu, Mwana wa Mtu naye atakiri mbele ya malaika wa Mungu kwamba mtu huyo ni wake.

9. Lakini, mtu yeyote anayenikana mbele ya watu, naye atakanwa mbele ya malaika wa Mungu.

10. “Yeyote anayesema neno la kumpinga Mwana wa Mtu atasamehewa; lakini anayemkufuru Roho Mtakatifu hatasamehewa.

11. “Watakapowapeleka nyinyi mbele ya masunagogi na mbele ya wakuu na watawala, msiwe na wasiwasi juu ya jinsi mtakavyojitetea au jinsi mtakavyosema.

12. Kwa maana wakati huo Roho Mtakatifu atawafundisheni kile mnachopaswa kusema.”

13. Mtu mmoja katika ule umati wa watu akamwambia, “Mwalimu, mwambie ndugu yangu tugawane urithi aliotuachia baba.”

14. Yesu akamjibu, “Rafiki, ni nani aliyeniweka mimi kuwa mwamuzi au msuluhishi kati yenu?”

15. Basi, akawaambia wote, “Jihadharini na kila aina ya tamaa; maana uhai wa mtu hautegemei wingi wa vitu alivyo navyo.”

Kusoma sura kamili Luka 12