Agano la Kale

Agano Jipya

Luka 12:22-38 Biblia Habari Njema (BHN)

22. Kisha Yesu akawaambia wanafunzi wake, “Kwa sababu hiyo nawaambieni, msiwe na wasiwasi juu ya chakula mnachohitaji ili kuishi, wala juu ya mavazi mnayohitaji kwa ajili ya miili yenu.

23. Kwa sababu uzima ni bora kuliko chakula, na mwili ni bora kuliko mavazi.

24. Chukueni kwa mfano, kunguru: Hawapandi, hawavuni wala hawana ghala yoyote. Hata hivyo, Mungu huwalisha. Nyinyi mna thamani zaidi kuliko ndege!

25. Ni nani kati yenu kwa kuwa na wasiwasi sana anaweza kuongeza kidogo urefu wa maisha yake?

26. Basi, kama hamwezi kufanya jambo dogo kama hilo, kwa nini kuwa na wasiwasi juu ya yale mengine?

27. Angalieni maua jinsi yanavyomea. Hayafanyi kazi wala hayafumi. Lakini nawaambieni, hata Solomoni mwenyewe na fahari zake zote hakupata kuvikwa vizuri kama ua mojawapo.

28. Ikiwa basi, Mungu hulivika hivyo jani la shambani ambalo leo liko na kesho latupwa motoni, je, si atawafanyia nyinyi zaidi? Enyi watu wenye imani haba!

29. “Basi, msivurugike akili, mkihangaika juu ya mtakachokula au mtakachokunywa.

30. Kwa maana hayo yote yanahangaikiwa na watu wote wasiomjua Mungu. Baba yenu anajua kwamba mnahitaji vitu hivyo.

31. Shughulikeni kwanza juu ya ufalme wa Mungu, na hayo mtapewa kwa ziada.

32. “Msiogope, enyi kundi dogo! Maana Baba yenu amependa kuwapeni ufalme.

33. Uzeni mali yenu mkawape maskini hizo fedha. Jifanyieni mifuko isiyochakaa, na kujiwekea hazina mbinguni ambako haitapungua. Huko wezi hawakaribii, wala nondo hawaharibu.

34. Pale ilipo hazina yako, ndipo pia utakapokuwa moyo wako.

35. “Muwe tayari mmejifunga mkanda kiunoni, na taa zenu ziwe zinawaka;

36. muwe kama watumishi wanaomngojea bwana wao arudi kutoka harusini, ili wamfungulie mara atakapobisha.

37. Heri yao watumishi wale ambao bwana wao atakaporudi atawakuta wanakesha! Nawaambieni hakika, huyo bwana atajifunga mkanda kiunoni, atawaketisha mezani na kuwahudumia.

38. Hata kama atarudi usiku wa manane au alfajiri na kuwakuta wanakesha, heri yao watumishi hao!

Kusoma sura kamili Luka 12