Agano la Kale

Agano Jipya

Luka 12:10-28 Biblia Habari Njema (BHN)

10. “Yeyote anayesema neno la kumpinga Mwana wa Mtu atasamehewa; lakini anayemkufuru Roho Mtakatifu hatasamehewa.

11. “Watakapowapeleka nyinyi mbele ya masunagogi na mbele ya wakuu na watawala, msiwe na wasiwasi juu ya jinsi mtakavyojitetea au jinsi mtakavyosema.

12. Kwa maana wakati huo Roho Mtakatifu atawafundisheni kile mnachopaswa kusema.”

13. Mtu mmoja katika ule umati wa watu akamwambia, “Mwalimu, mwambie ndugu yangu tugawane urithi aliotuachia baba.”

14. Yesu akamjibu, “Rafiki, ni nani aliyeniweka mimi kuwa mwamuzi au msuluhishi kati yenu?”

15. Basi, akawaambia wote, “Jihadharini na kila aina ya tamaa; maana uhai wa mtu hautegemei wingi wa vitu alivyo navyo.”

16. Kisha akawaambia mfano: “Kulikuwa na tajiri mmoja ambaye shamba lake lilizaa mavuno mengi.

17. Tajiri huyo akafikiri moyoni mwake: ‘Nitafanyaje nami sina mahali pa kuhifadhia mavuno yangu?

18. Nitafanya hivi: Nitabomoa ghala zangu na kujenga kubwa zaidi, nami nitahifadhi humo mavuno yangu yote na mali yangu.

19. Hapo nitaweza kuiambia roho yangu: Sasa unayo akiba ya matumizi kwa miaka na miaka. Ponda mali, kula, kunywa na kufurahi.’

20. Lakini Mungu akamwambia: ‘Mpumbavu wewe; leo usiku roho yako itachukuliwa. Na vitu vile vyote ulivyojirundikia vitakuwa vya nani?’”

21. Yesu akamaliza kwa kusema, “Ndivyo ilivyo kwa mtu anayejirundikia mali kwa ajili yake mwenyewe, lakini si tajiri mbele ya Mungu.”

22. Kisha Yesu akawaambia wanafunzi wake, “Kwa sababu hiyo nawaambieni, msiwe na wasiwasi juu ya chakula mnachohitaji ili kuishi, wala juu ya mavazi mnayohitaji kwa ajili ya miili yenu.

23. Kwa sababu uzima ni bora kuliko chakula, na mwili ni bora kuliko mavazi.

24. Chukueni kwa mfano, kunguru: Hawapandi, hawavuni wala hawana ghala yoyote. Hata hivyo, Mungu huwalisha. Nyinyi mna thamani zaidi kuliko ndege!

25. Ni nani kati yenu kwa kuwa na wasiwasi sana anaweza kuongeza kidogo urefu wa maisha yake?

26. Basi, kama hamwezi kufanya jambo dogo kama hilo, kwa nini kuwa na wasiwasi juu ya yale mengine?

27. Angalieni maua jinsi yanavyomea. Hayafanyi kazi wala hayafumi. Lakini nawaambieni, hata Solomoni mwenyewe na fahari zake zote hakupata kuvikwa vizuri kama ua mojawapo.

28. Ikiwa basi, Mungu hulivika hivyo jani la shambani ambalo leo liko na kesho latupwa motoni, je, si atawafanyia nyinyi zaidi? Enyi watu wenye imani haba!

Kusoma sura kamili Luka 12