Agano la Kale

Agano Jipya

Luka 11:33-49 Biblia Habari Njema (BHN)

33. “Hakuna mtu anayewasha taa na kuifunika kwa debe, bali huiweka juu ya kinara ili watu wanaoingia ndani wapate kuona mwanga.

34. Jicho lako ni taa ya mwili wako; likiwa zima, mwili wako wote utakuwa katika mwanga. Jicho lako likiwa bovu, na mwili wako pia utakuwa katika giza.

35. Uwe mwangalifu basi, mwanga ulio ndani yako usije ukawa giza.

36. Basi, kama mwili wako wote una mwanga, bila kuwa na sehemu yoyote yenye giza, mwili huo utangaa kikamilifu kama vile taa inavyokuangazia kwa mwanga wake.”

37. Yesu alipokuwa akiongea, Mfarisayo mmoja alimkaribisha chakula nyumbani kwake, naye akaenda, akaketi kula chakula.

38. Huyo Mfarisayo alistaajabu kuona kwamba alikula chakula bila kunawa kwanza.

39. Bwana akamwambia, “Nyinyi Mafarisayo huosha kikombe na sahani kwa nje, lakini ndani mmejaa udhalimu na uovu.

40. Wapumbavu nyinyi! Je, aliyetengeneza nje si ndiye aliyetengeneza ndani pia?

41. Toeni kwa maskini vile vitu vilivyomo ndani, na vingine vyote vitakuwa halali kwenu.

42. “Lakini ole wenu Mafarisayo, kwa sababu mnatoza watu zaka hata juu ya majani ya kukolezea chakula, mchicha na majani mengine, na huku hamjali juu ya haki na upendo kwa Mungu. Mambo haya iliwapasa muwe mmeyazingatia bila kuyasahau yale mengine.

43. “Ole wenu nyinyi Mafarisayo, kwa sababu mnapenda kuketi mbele mahali pa heshima katika masunagogi, na kusalimiwa kwa heshima hadharani.

44. Ole wenu, kwa sababu mko kama makaburi yaliyofichika; watu hutembea juu yake bila kufahamu.”

45. Mmoja wa waalimu wa sheria akamwambia, “Mwalimu, maneno yako yanatukashifu na sisi pia.”

46. Yesu akamjibu, “Na nyinyi waalimu wa sheria, ole wenu; maana mnawatwika watu mizigo isiyochukulika, huku nyinyi wenyewe hamnyoshi hata kidole kuwasaidia.

47. Ole wenu, kwa kuwa mnajenga makaburi ya manabii wale ambao wazee wenu waliwaua.

48. Kwa hiyo mnashuhudia na kukubaliana na matendo ya wazee wenu; maana wao waliwaua hao manabii, nanyi mnajenga makaburi yao.

49. Kwa hiyo, Hekima ya Mungu ilisema hivi: ‘Nitawapelekea manabii na mitume, lakini watawaua baadhi yao, na kuwatesa wengine.’

Kusoma sura kamili Luka 11