Agano la Kale

Agano Jipya

Luka 1:1-15 Biblia Habari Njema (BHN)

1. Mheshimiwa Theofilo: Watu wengi wamejitahidi kuandika juu ya mambo yale yaliyotendeka kati yetu.

2. Waliyaandika kama tulivyoelezwa na wale walioyaona mambo hayo kwa macho yao tangu mwanzo, na waliotangaza ujumbe huo.

3. Inafaa nami pia, Mheshimiwa, baada ya kuchunguza kwa makini mambo yote tangu mwanzo, nikuandikie kwa mpango,

4. ili nawe uweze kujionea mwenyewe ukweli wa mambo yale uliyofundishwa.

5. Wakati Herode alipokuwa mfalme wa Yudea, kulikuwa na kuhani mmoja jina lake Zakaria, wa kikundi cha ukuhani cha Abiya. Mke wake alikuwa anaitwa Elisabeti, naye alikuwa wa ukoo wa kuhani Aroni.

6. Wote wawili walikuwa wanyofu mbele ya Mungu, wakiishi kwa kufuata amri na maagizo yote ya Bwana bila lawama.

7. Lakini hawakuwa wamejaliwa watoto kwa vile Elisabeti alikuwa tasa, nao wote wawili walikuwa wazee sana.

8. Siku moja, ilipokuwa zamu yake kutoa huduma ya ukuhani mbele ya Mungu,

9. Zakaria alichaguliwa kwa kura, kama ilivyokuwa desturi, kuingia hekaluni ili afukize ubani.

10. Watu, umati mkubwa, walikuwa wamekusanyika nje wanasali wakati huo wa kufukiza ubani.

11. Malaika wa Bwana akamtokea humo ndani, akasimama upande wa kulia wa madhabahu ya kufukizia ubani.

12. Zakaria alipomwona alifadhaika, hofu ikamwingia.

13. Lakini malaika akamwambia, “Zakaria, usiogope, kwa maana sala yako imesikilizwa, na Elisabeti mkeo atakuzalia mtoto wa kiume, nawe utampa jina Yohane.

14. Utakuwa na furaha kubwa na watu wengi watashangilia kwa sababu ya kuzaliwa kwake.

15. Atakuwa mkubwa mbele ya Bwana. Hatakunywa divai wala kileo, atajazwa Roho Mtakatifu tangu tumboni mwa mama yake.

Kusoma sura kamili Luka 1