Agano la Kale

Agano Jipya

2 Wakorintho 8:10-20 Biblia Habari Njema (BHN)

10. Kuhusu jambo hili, basi, nawapeni shauri hili: Inafaa kwenu kutekeleza sasa yale mliyoanza mwaka jana. Nyinyi mlikuwa wa kwanza kuchukua hatua na kuamua kufanya hivyo.

11. Basi, kamilisheni shughuli hiyo; na kama vile mlivyokuwa na hamu kubwa ya kusaidia, basi, fanyeni bidii vivyo hivyo, kadiri ya uwezo wenu, kuikamilisha.

12. Maana ikiwa mtu ana moyo wa kusaidia, Mungu hupokea kila anachoweza kutoa; hadai zaidi.

13. Nyinyi hampaswi kuongezewa taabu kusudi wengine wapunguziwe mzigo wao; sivyo, ila ni lazima tujali usawa na haki.

14. Kila mlicho nacho sasa cha ziada kiwasaidie wale wanaohitaji, ili nao wakati watakapokuwa na ziada, wawasaidie nyinyi katika mahitaji yenu, na hivyo kuwe na usawa.

15. Kama Maandiko yasemavyo:“Aliyekusanya kwa wingi hakuwa na ziada,na yule aliyekusanya kidogo hakupungukiwa.”

16. Namshukuru Mungu aliyeweka ndani ya moyo wa Tito hamu hiyo niliyo nayo mimi ya kuwasaidia.

17. Si tu kwamba alikubali ombi letu, ila pia alikuwa na hamu kubwa ya kusaidia, hata akaamua kwa hiari yake mwenyewe kuja kwenu.

18. Pamoja naye, tunamtuma ndugu mmoja ambaye sifa zake katika kueneza Injili zimeenea katika makanisa yote.

19. Zaidi ya hayo, yeye amechaguliwa na makanisa awe mwenzetu safarini wakati tunapopeleka huduma hii yetu ya upendo, huduma tunayoifanya kwa ajili ya utukufu wa Bwana na uthibitisho wa nia yetu njema.

20. Tunataka kuepa lawama zinazoweza kutokea kuhusu usimamizi wetu juu ya zawadi hii karimu.

Kusoma sura kamili 2 Wakorintho 8