Agano la Kale

Agano Jipya

2 Wakorintho 5:2-12 Biblia Habari Njema (BHN)

2. Na sasa, katika hali hii, tunaugua tukitazamia kwa hamu kubwa kuvikwa makao yetu yaliyo mbinguni.

3. Naam, tunapaswa kuvikwa namna hiyo ili tusije tukasimama mbele ya Mungu bila vazi.

4. Tukiwa bado katika hema hii ya duniani, tunalia kwa kukandamizwa; si kwamba tunataka kuuvua mwili huu wa kufa, ila tuna hamu ya kuvalishwa ule usiokufa, ili kile chenye kufa kimezwe kabisa na uhai.

5. Mungu mwenyewe alitutayarishia mabadiliko hayo, naye ametupa Roho wake awe dhamana ya yote aliyotuwekea.

6. Tuko imara daima. Tunajua kwamba kuishi katika mwili huu tu ni kukaa mbali na Bwana.

7. Maana tunaishi kwa imani, na si kwa kuona.

8. Lakini tuko imara na tungependelea hata kuyahama makao haya, tukahamie kwa Bwana.

9. Lakini jambo la maana zaidi, tunataka kumpendeza, iwe tunaishi hapa duniani au huko.

10. Maana sote ni lazima tusimame mbele ya kiti cha hukumu cha Kristo, ili kila mmoja apokee anayostahili kwa matendo aliyoyafanya wakati alipokuwa anaishi duniani, mema au mabaya.

11. Basi, sisi tunajua umuhimu wa kumcha Bwana, na hivyo tunajitahidi kuwavuta watu. Mungu anatujua waziwazi, nami natumaini kwamba nanyi pia mnatujua kinaganaga.

12. Si kwamba tunajaribu tena kujipendekeza kwenu, ila tunataka kuwapa nyinyi sababu zetu za kuona fahari juu yenu, ili mpate kuwajibu wale wanaojivunia hali yao ya nje zaidi kuliko jinsi walivyo moyoni.

Kusoma sura kamili 2 Wakorintho 5