Agano la Kale

Agano Jipya

2 Wakorintho 11:16-30 Biblia Habari Njema (BHN)

16. Tena nasema: Mtu asinifikirie kuwa mpumbavu. Lakini kama mkifikiri hivyo, basi, nichukueni kama mpumbavu ili nami nipate kuwa na cha kujivunia angaa kidogo.

17. Ninachosema sasa si kile alichoniagiza Bwana; kuhusu jambo hili la kujivuna, nasema tu kama mtu mpumbavu.

18. Maadamu wengi hujivuna kwa sababu za kidunia, nami pia nitajivuna.

19. Nyinyi ni wenye busara, ndiyo maana hata mnawavumilia wapumbavu!

20. Mnamvumilia hata mtu anayewafanya nyinyi watumwa, mtu mwenye kuwanyonya, mwenye kuwakandamiza, mwenye kuwadharau na kuwapiga usoni!

21. Kwa aibu nakubali kwamba sisi tulikuwa dhaifu.Iwe iwavyo, lakini kama kuna mtu yeyote anayethubutu kujivunia kitu – nasema kama mtu mpumbavu – mimi nathubutu pia.

22. Je, wao ni Waebrania? Hata mimi. Je, wao ni Waisraeli? Hata mimi. Wao ni wazawa wa Abrahamu? Hata mimi.

23. Wao ni watumishi wa Kristo? Hata mimi – nanena hayo kiwazimu – ni mtumishi wa Kristo zaidi kuliko wao. Mimi nimefanya kazi ngumu zaidi, nimekaa gerezani mara nyingi zaidi, nimepigwa mara nyingi zaidi na nimekaribia kifo mara nyingi.

24. Mara tano nilichapwa vile viboko arubaini kasoro kimoja vya Wayahudi.

25. Nilipigwa fimbo mara tatu, nilipigwa mawe mara moja; mara tatu nilivunjikiwa meli baharini, na humo nikakesha usiku kucha na kushinda mchana kutwa.

26. Kila mara safarini nimekabiliwa na hatari za mafuriko ya mito, na hatari za wanyama; hatari kutoka kwa wananchi wenzangu na kutoka kwa watu wa mataifa mengine; hatari za mjini, hatari za porini, hatari za baharini, hatari kutoka kwa ndugu wa uongo.

27. Nimefanya kazi na kutaabika, nimekesha bila usingizi mara nyingi; nimekuwa na njaa na kiu; mara nyingi nimefunga na kukaa katika baridi bila nguo.

28. Na, licha ya mengine mengi, kila siku nakabiliwa na shughuli za makanisa yote.

29. Kama mtu yeyote ni dhaifu, nami pia ni dhaifu; mtu yeyote akikwazwa, nami pia huwa na wasiwasi.

30. Ikinilazimu kujivuna, basi, nitajivunia udhaifu wangu.

Kusoma sura kamili 2 Wakorintho 11