Agano la Kale

Agano Jipya

1 Wakorintho 9:6-18 Biblia Habari Njema (BHN)

6. Au ni mimi tu na Barnaba ambao tunapaswa kujipatia maslahi yetu kwa kufanya kazi?

7. Je, mwanajeshi gani anayelipia utumishi wake jeshini? Mkulima gani asiyekula matunda ya shamba lake la mizabibu? Mchungaji gani asiyekunywa maziwa ya mifugo yake?

8. Je, nasema mambo haya kibinadamu tu? Je, sheria nayo haisemi hivyo?

9. Imeandikwa katika sheria: “Usimfunge kinywa ng'ombe anapopura nafaka.” Je, ndio kusema Mungu anajishughulisha na ng'ombe?

10. Je, hakuwa anatufikiria sisi aliposema hivyo? Naam, haya yaliandikwa kwa ajili yetu; maana yule anayelima na yule anayevuna, wote wawili wana haki ya kutumaini kupata sehemu ya mavuno.

11. Ikiwa sisi tumepanda mbegu ya kiroho kati yenu, je, ni jambo kubwa tukichuma kwenu faida ya kidunia?

12. Ikiwa wengine wanayo haki ya kutazamia hayo kutoka kwenu, je, sisi hatuna haki zaidi kuliko hao?Lakini, sisi hatukuitumia haki hiyo. Badala yake, tumestahimili kila kitu ili tusiiwekee kizuizi chochote Habari Njema ya Kristo.

13. Je, hamjui kwamba wanaotumikia hekaluni hupata chakula chao hekaluni, na kwamba wanaotoa sadaka madhabahuni hupata sehemu ya hiyo sadaka?

14. Bwana aliagiza vivyo hivyo; wahubiri wa Habari Njema wapate riziki zao kutokana nayo.

15. Lakini, mimi sikutumia hata mojawapo ya haki hizo. Na wala siandiki nijipatie haki hizo; kwangu mimi ni afadhali kufa kuliko kumfanya yeyote aone kwamba najisifu bure.

16. Ikiwa ninaihubiri injili, hilo si jambo la kujivunia; hilo ni jukumu nililopewa. Na, ole wangu kama sitaihubiri injili!

17. Ningekuwa nimeichagua kazi hii kwa hiari, basi, ningetazamia malipo; lakini maadamu naifanya ikiwa ni wajibu, hiyo ina maana kwamba ni jukumu nililopewa nitekeleze.

18. Mshahara wangu ni kitu gani, basi? Mshahara wangu ni fursa ya kuihubiri Habari Njema bure, bila kudai haki ninazostahili kwa kuihubiri.

Kusoma sura kamili 1 Wakorintho 9