Agano la Kale

Agano Jipya

1 Wakorintho 4:1-11 Biblia Habari Njema (BHN)

1. Mtu na atuone sisi kuwa ni watumishi wa Kristo tuliokabidhiwa siri za Mungu.

2. Kinachotakiwa kwa yeyote yule aliyekabidhiwa kazi ni kuwa mwaminifu.

3. Kwangu mimi si kitu nikihukumiwa na nyinyi, au na mahakama ya kibinadamu; wala sijihukumu mimi mwenyewe.

4. Dhamiri yangu hainishtaki kwa jambo lolote, lakini hiyo haionyeshi kwamba sina lawama. Bwana ndiye anayenihukumu.

5. Basi, msihukumu kabla ya wakati wake; acheni mpaka Bwana atakapokuja. Yeye atayafichua mambo ya giza yaliyofichika, na kuonesha wazi nia za mioyo ya watu. Ndipo kila mmoja atapata sifa anayostahili kutoka kwa Mungu.

6. Ndugu, hayo yote niliyosema juu ya Apolo na juu yangu, ni kielelezo kwenu: Kutokana na mfano wangu mimi na Apolo nataka mwelewe maana ya msemo huu: “Zingatieni yaliyoandikwa.” Kati yenu pasiwe na mtu yeyote anayejivunia mtu mmoja na kumdharau mwingine.

7. Nani amekupendelea wewe? Una kitu gani wewe ambacho hukupewa? Na ikiwa umepewa, ya nini kujivunia kana kwamba hukukipewa?

8. Haya! Mmekwisha shiba! Mmekwisha kuwa matajiri! Mmekuwa wafalme bila ya sisi! Naam, laiti mngekuwa kweli watawala, ili nasi pia tutawale pamoja nanyi.

9. Nafikiri Mungu ametufanya sisi mitume tuwe watu wa mwisho kabisa, kama watu waliohukumiwa kuuawa, maana tumekuwa tamasha mbele ya ulimwengu wote, mbele ya malaika na watu.

10. Sisi ni wapumbavu kwa ajili ya Kristo, lakini nyinyi ni wenye busara katika kuungana na Kristo! Sisi ni dhaifu, nyinyi ni wenye nguvu. Nyinyi mnaheshimika, sisi tunadharauliwa.

11. Mpaka dakika hii, sisi tuna njaa na kiu, hatuna nguo, twapigwa makofi, hatuna malazi.

Kusoma sura kamili 1 Wakorintho 4