Agano la Kale

Agano Jipya

1 Wakorintho 15:45-55 Biblia Habari Njema (BHN)

45. Maana Maandiko yasema: “Mtu wa kwanza, Adamu, alikuwa kiumbe mwenye uhai;” lakini Adamu wa mwisho ni Roho awapaye watu uhai.

46. Lakini unaotangulia kuwako si ule mwili wa kiroho, ila ule mwili wa kawaida, kisha ule mwili wa kiroho.

47. Adamu wa kwanza aliumbwa kwa udongo, alitoka ardhini; mtu wa pili alitoka mbinguni.

48. Wote walio wa dunia wako kama huyo mtu aliyeumbwa kwa udongo; wale walio wa mbinguni wako kama yule aliyetoka mbinguni.

49. Kama vile tulivyofanana na yule aliyeumbwa kwa udongo, vivyo hivyo tutafanana na huyo aliyetoka mbinguni.

50. Basi, ndugu, nasema hivi: Kile kilichofanywa kwa mwili na damu hakiwezi kuushiriki ufalme wa Mungu; na chenye kuharibika hakiwezi kuwa na hali ya kutoharibika.

51. Sikilizeni, nawaambieni siri: Sisi hatutakufa sote, ila sote tutageuzwa,

52. wakati wa mbiu ya mwisho, kwa nukta moja, kufumba na kufumbua. Maana tarumbeta ya mwisho itakapolia, wafu watafufuliwa katika hali ya kutoweza kufa tena, na sisi tutageuzwa.

53. Maana ni lazima kila kiharibikacho kijivalie hali ya kutoharibika, mwili uwezao kufa ujivalie hali ya kutokufa.

54. Basi, mwili huu wenye kuharibika utakapojivalia hali ya kutoharibika, na kile chenye kufa kitakapojivalia hali ya kutokufa, hapo ndipo litakapotimia lile neno lililoandikwa: “Kifo kimeangamizwa; ushindi umekamilika!”

55. “Kifo, ushindi wako uko wapi?Uwezo wako wa kuumiza uko wapi?”

Kusoma sura kamili 1 Wakorintho 15