Agano la Kale

Agano Jipya

1 Wakorintho 15:1-16 Biblia Habari Njema (BHN)

1. Sasa, ndugu, napenda kuwakumbusha ile Habari Njema niliyowahubirieni, nanyi mkaipokea na kusimama imara ndani yake.

2. Kwa njia yake mnaokolewa, ikiwa mnayazingatia maneno niliyowahubirieni, na kama kuamini kwenu hakukuwa bure.

3. Mimi niliwakabidhi nyinyi mambo muhimu sana ambayo mimi niliyapokea: Kwamba Kristo alikufa kwa ajili ya dhambi zetu kufuatana na Maandiko Matakatifu;

4. kwamba alizikwa, akafufuka siku ya tatu kufuatana na Maandiko Matakatifu;

5. kwamba alimtokea Kefa, na baadaye aliwatokea wale kumi na wawili.

6. Kisha aliwatokea ndugu zaidi ya 500 kwa mara moja; wengi wao wanaishi bado, lakini baadhi yao wamekwisha kufa.

7. Baadaye alimtokea Yakobo kisha akawatokea mitume wote.

8. Baada ya wote, akanitokea hata mimi, mimi niliyekuwa kama mtu aliyezaliwa kabla ya wakati.

9. Maana mimi ni mdogo kabisa miongoni mwa mitume, na wala sistahili kuitwa mtume, kwa sababu nililidhulumu kanisa la Mungu.

10. Lakini, kwa neema yake Mungu, nimekuwa kama nilivyo, na neema yake kwangu haikuwa bure. Mimi nimefanya kazi kuliko wote; si mimi hasa, ila ni neema ya Mungu ifanyayo kazi pamoja nami.

11. Lakini hata hivyo, iwe wao ndio wahubirio au mimi nihubiriye, haidhuru, hiki ndicho tunachohubiri, na hiki ndicho mnachoamini.

12. Sasa, maadamu inahubiriwa kwamba Kristo amefufuliwa kutoka kwa wafu, baadhi yenu wanawezaje kusema kwamba hakuna ufufuo wa wafu?

13. Kama hakuna ufufuo wa wafu, basi, Kristo naye hakufufuka;

14. na kama Kristo hakufufuka, basi mahubiri yetu hayana maana na imani yenu haina maana.

15. Zaidi ya hayo sisi tungekuwa mashahidi wa uongo mbele ya Mungu, maana tulisema kwamba Mungu alimfufua Kristo kutoka kwa wafu na kumbe yeye hakumfufua – kama ni kweli kwamba wafu hawafufuliwi.

16. Maana, ikiwa ni kweli kwamba wafu hawafufuki, basi naye Kristo hakufufuka.

Kusoma sura kamili 1 Wakorintho 15