Agano la Kale

Agano Jipya

1 Wakorintho 12:2-18 Biblia Habari Njema (BHN)

2. Mnajua kwamba, kabla ya kuongoka kwenu, mlitawaliwa na kupotoshwa na sanamu tupu.

3. Basi, jueni kwamba mtu yeyote anayeongozwa na Roho wa Mungu hawezi kusema: “Yesu alaaniwe!” Hali kadhalika, mtu yeyote hawezi kusema: “Yesu ni Bwana,” asipoongozwa na Roho Mtakatifu.

4. Vipaji vya kiroho ni vya namna nyingi, lakini Roho avitoaye ni mmoja.

5. Kuna namna nyingi za kutumikia, lakini Bwana anayetumikiwa ni mmoja.

6. Kuna namna mbalimbali za kufanya kazi ya huduma, lakini Mungu ni mmoja, anayewezesha kazi zote katika wote.

7. Kila mtu hupewa mwangaza wa Roho kwa faida ya wote.

8. Roho humpa mmoja ujumbe wa hekima, na mwingine ujumbe wa elimu, apendavyo Roho huyohuyo.

9. Roho huyohuyo humpa mmoja imani, na humpa mwingine kipaji cha kuponya;

10. humpa mmoja kipaji cha kufanya miujiza, mwingine kipaji cha kusema ujumbe wa Mungu, mwingine kipaji cha kubainisha vipaji vitokavyo kwa Roho na visivyo vya Roho; humpa mmoja kipaji cha kusema lugha ngeni, na mwingine kipaji cha kuzifafanua.

11. Hizo zote ni kazi za Roho huyohuyo mmoja, ambaye humpa kila mtu kipaji tofauti, kama apendavyo mwenyewe.

12. Kama vile mwili ulivyo mmoja wenye viungo vingi, na viungo hivyo vyote – ingawaje ni vingi – hufanya mwili mmoja, ndivyo ilivyo pia kwa Kristo.

13. Maana sisi, tukiwa Wayahudi au watu wa mataifa mengine, watumwa au watu huru, sote tumebatizwa kwa Roho mmoja katika mwili huo mmoja; na sote tukanyweshwa Roho huyo mmoja.

14. Mwili hauna kiungo kimoja tu, bali una viungo vingi.

15. Kama mguu ungejisemea: “Kwa kuwa mimi si mkono, basi mimi si mali ya mwili,” je, ungekoma kuwa sehemu ya mwili? La hasha!

16. Kama sikio lingejisemea: “Kwa vile mimi si jicho, basi mimi si mali ya mwili,” je, kwa hoja hiyo lingekoma kuwa sehemu ya mwili? La!

17. Kama mwili wote ungekuwa jicho, sikio lingekuwa wapi? Na kama mwili wote ungekuwa sikio, mtu angewezaje kunusa?

18. Lakini kama ilivyo, Mungu alizipanga sehemu hizo tofauti katika mwili kama alivyopenda.

Kusoma sura kamili 1 Wakorintho 12