Agano la Kale

Agano Jipya

1 Wakorintho 10:18-33 Biblia Habari Njema (BHN)

18. Angalieni kwa mfano Wayahudi wenyewe: Wale wanaokula tambiko wanaungana na hiyo madhabahu.

19. Nataka kusema nini, basi? Kwamba chakula kilichotambikiwa sanamu ni kitu zaidi ya chakula? Na hizo sanamu, je, ni kitu kweli zaidi ya sanamu?

20. Hata kidogo! Ninachosema ni kwamba tambiko wanazotoa watu wasiomjua Mungu wanawatolea pepo, sio Mungu. Sipendi kamwe nyinyi muwe na ushirika na pepo.

21. Hamwezi kunywa kikombe cha Bwana na kikombe cha pepo; hamwezi kushiriki katika Karamu ya Bwana na katika meza ya pepo.

22. Au je, tunataka kumfanya Bwana awe na wivu? Mnadhani tuna nguvu zaidi kuliko yeye?

23. Vitu vyote ni halali, lakini si vyote vinafaa. Vitu vyote ni halali lakini si vyote vinajenga.

24. Mtu asitafute faida yake mwenyewe, ila faida ya mwenzake.

25. Kuleni chochote kile kiuzwacho sokoni bila ya kuulizauliza kwa sababu ya dhamiri zenu;

26. maana Maandiko yasema: “Dunia na vyote vilivyomo ni mali ya Bwana.”

27. Kama mtu ambaye si mwaamini akiwaalikeni nanyi mkakubali kwenda, basi, kuleni vyote atakavyowaandalieni bila kuulizauliza kwa sababu ya dhamiri zenu.

28. Lakini mtu akiwaambieni: “Chakula hiki kimetambikiwa sanamu,” basi, kwa ajili ya huyo aliyewaambieni hivyo na kwa ajili ya dhamiri, msile.

29. Nasema, “kwa ajili ya dhamiri,” si dhamiri yenu, bali dhamiri yake huyo aliyewaambieni.Mtaniuliza: “Kwa nini uhuru wangu utegemee dhamiri ya mtu mwingine?

30. Ikiwa mimi nashiriki chakula hicho huku namshukuru Mungu, kwa nini nilaumiwe kwa chakula ambacho kwa ajili yake nimemshukuru Mungu?”

31. Basi, chochote mfanyacho iwe ni kula au kunywa, fanyeni yote kwa ajili ya utukufu wa Mungu.

32. Msiwe kikwazo kwa Wayahudi au kwa Wagiriki au kwa kanisa la Mungu.

33. Muwe kama mimi; najaribu kuwapendeza wote kwa kila njia, bila kutafuta faida yangu mwenyewe ila faida ya wote, wapate kuokolewa.

Kusoma sura kamili 1 Wakorintho 10