Agano la Kale

Agano Jipya

1 Wakorintho 1:1-12 Biblia Habari Njema (BHN)

1. Mimi Paulo, niliyeitwa kuwa mtume wa Kristo Yesu kwa mapenzi ya Mungu, na ndugu Sosthene,

2. tunawaandikia nyinyi mlio kanisa la Mungu huko Korintho. Nyinyi mmefanywa watakatifu katika kuungana na Kristo Yesu, mkaitwa muwe watu wa Mungu, pamoja na watu wote popote wanaomwomba Bwana wetu Yesu Kristo aliye Bwana wao na wetu pia.

3. Nawatakieni neema na amani kutoka kwa Mungu Baba yetu na Bwana wetu Yesu Kristo.

4. Ninamshukuru Mungu wangu daima kwa ajili yenu kwa sababu amewatunukia nyinyi neema yake kwa njia ya Kristo Yesu.

5. Maana, kwa kuungana na Kristo mmetajirishwa katika kila kitu. Mmejaliwa elimu yote na uwezo wote wa kuhubiri.

6. Maana ujumbe juu ya Kristo umethibitishwa ndani yenu,

7. hata hampungukiwi kipaji chochote cha kiroho mkiwa mnangojea kufunuliwa kwake Bwana wetu Yesu Kristo.

8. Yeye atawaimarisheni nyinyi mpaka mwisho mpate kuonekana bila hatia siku ile ya Bwana wetu Yesu Kristo.

9. Mungu ni mwaminifu; yeye aliwaita nyinyi muwe na umoja na Mwanae Yesu Kristo Bwana wetu.

10. Ndugu, nawasihini kwa jina la Bwana wetu Yesu Kristo: Pataneni nyote katika kila jambo msemalo; yasiweko mafarakano kati yenu; muwe na fikira moja na nia moja.

11. Ndugu zangu, habari nilizopata kutoka kwa watu kadhaa wa jamaa ya Kloe, zaonesha wazi kwamba kuna kutoelewana kati yenu.

12. Nataka kusema hivi: Kila mmoja anasema chake: Mmoja husema, “Mimi ni wa Paulo”, mwingine: “Mimi ni wa Apolo”, mwingine: “Mimi ni wa Kefa,” na mwingine: “Mimi ni wa Kristo.”

Kusoma sura kamili 1 Wakorintho 1