Agano la Kale

Agano Jipya

1 Petro 4:10-19 Biblia Habari Njema (BHN)

10. Kila mmoja anapaswa kutumia kipaji alichojaliwa na Mungu kwa faida ya wengine kama wakili mwema wa zawadi mbalimbali za Mungu.

11. Anayesema kitu, maneno yake na yawe kama maneno ya Mungu; anayetumikia anapaswa kutumikia kwa nguvu anayojaliwa na Mungu, ili katika mambo yote, Mungu atukuzwe kwa njia ya Yesu Kristo ambaye utukufu na nguvu ni vyake milele na milele! Amina.

12. Wapenzi wangu, msishangae kuhusu majaribio makali mnayopata kana kwamba mnapatwa na kitu kisicho cha kawaida.

13. Ila furahini kwamba mnashiriki mateso ya Kristo ili muweze kuwa na furaha tele wakati utukufu wake utakapofunuliwa.

14. Heri yenu ikiwa mnatukanwa kwa sababu ya jina la Kristo; jambo hilo lamaanisha kwamba Roho mtukufu, yaani Roho wa Mungu, anakaa nanyi.

15. Asiwepo mtu yeyote miongoni mwenu ambaye anapaswa kuteseka kwa sababu ni mwuaji, mwizi, mhalifu au mwovu.

16. Lakini kama mtu akiteseka kwa sababu ni Mkristo, basi, asione aibu, bali amtukuze Mungu, kwa sababu mtu huyo anaitwa kwa jina la Kristo.

17. Wakati wa hukumu umefika, na hukumu hiyo inaanza na watu wake Mungu mwenyewe. Ikiwa hukumu hiyo inaanzia kwetu sisi, basi, mwisho wake utakuwa namna gani kwa wale wasioamini Habari Njema ya Mungu?

18. Kama yasemavyo Maandiko Matakatifu:“Ni vigumu kwa watu waadilifu kuokolewa;itakuwaje basi, kwa wasiomcha Mungu na wenye dhambi?”

19. Kwa hiyo, wale wanaoteseka kufuatana na matakwa ya Mungu, wanapaswa, kwa matendo yao mema, kujiweka chini ya Muumba wao ambaye ni wa kuaminika kabisa.

Kusoma sura kamili 1 Petro 4